Serikali imesema, imeendelea kulipa hisa za umiliki katika Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki hadi kufikia dola za Marekani milioni 131.0 na tayari kibali cha kuanza ujenzi wa mradi huo kimetolewa Januari 2023.
Majaliwa ameyasema hayo leo hii leo Aprili 5, 2023 wakati akiwasilisha hotuba kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2023/2024 bungeni jijini Dodoma.
Amesema mradi mwingine unaotekelezwa kuwa ni ujenzi wa kiwanda cha sukari Mkulazi ambapo takribani Shilingi 39.84 Bilioni zimetolewa, ili kuendelea na ujenzi wa kiwanda ambao umefikia asilimia 75 na kuongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo hekta 219 zimepandwa miwa na kufanya ukubwa wa eneo lililopandwa miwa kufikia hekta 2,974, sawa na asilimia 83 ya lengo la kupanda hekta 3,600.
Bomba la Mafuta kati ya Tanzania na Uganda.
Aidha Majaliwa ameongeza kuwa, kiwanda hicho kinatarajiwa kuongeza uzalishaji wa tani 50,000 za sukari kwa mwaka pindi kitakapoanza uzalishaji na hivyo kupunguza mahitaji ya kuagiza sukari nje ya nchi na kwamba, “takribani shilingi bilioni 93.09 zimetolewa kuendelea na ujenzi mradi wa daraja la Kigongo-Busisi ambao umefikia asilimia 63 na kukamilika kwake kutapunguza muda wa wananchi kuvuka.”
Amesema, Daraja hilo litakapokamilika litapunguza muda wa wananchi kutoka eneo la Kigongo – Busisi kwa takribani muda wa saa mbili hadi dakika nne kwa kutumia usafiri wa gari na dakika 10 kwa watembea kwa Miguu na kwamba licha ya kupunguza muda wa kuvuka pia litakuwa na uwezo wa kupitisha magari ya aina yote wakati wote na kubeba uzito wa hadi tani 160.
Daraja la Kigongo – Busisi
Ameitaja miradi mingine kuwa ni ujenzi na ukarabati wa viwanja vya vdege, ambapo Serikali ilitoa takribani shilingi bilioni 77.23 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ambapo utekelezaji umefikia asilimia 10.2.
Aidha, kazi nyingine ni kukamilika kwa upanuzi wa njia ya kutua na kuruka ndege na kufungwa kwa mfumo wa kuongozea ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Dodoma; kukamilika kwa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Geita; na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa Viwanja vya ndege vya Songea kwa asilimia 98, Iringa asilimia 42 na Musoma asilimia 43.