Harbinder Singh Sethi, aliyekuwa kigogo wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), jana alilalamika mahakamani akiomba kuruhusiwa kuzungumza na mkewe ambaye anadai hajawahi kuzungumza naye kwa miezi sita.
Sethi alitoa malalamiko hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Kisutu, Huruma Shaidi baada ya mwanasheria wa serikali, Mwanaamina Kimakono kuiomba mahakama hiyo kuahirisha kesi hiyo kwani upelelezi bado haujakamilika.
Wakili wake, Dola Mallaba aliiambia mahakama hiyo kuwa tangu aliposhikiliwa, uongozi wa gereza la Ukonga umemnyima ruhusa ya kuonana na mkewe, hivyo anaiomba mahakama hiyo kumpa angalau dakika tano mteja wake azungumze na mkewe ambaye alikuwa mahakamani hapo.
Hata hivyo, Hakimu Shaidi alitupilia mbali ombi hilo akieleza kuwa uamuzi wa kumruhusu kuzungumza na familia yake ni wa jeshi la magereza.
“Kama kuna tatizo lolote juu ya hilo, mnapaswa kuliwasilisha hapa mahakamani,” alisema Hakimu Shaidi na kuahirisha kesi hiyo.
Sethi anashikiliwa kwenye gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha, kughushi pamoja na kuisababishia Serikali hasara ya Sh350 bilioni.