Mshambuliaji kutoka nchini Ghana na klabu ya Namungo FC Steven Sey, ametumia msemo wa Kiingereza usemao, “What goes around comes around,” akiwa na maana kwamba, kile ambacho alikuwa akikifanya pindi ambapo alikuwa akiwatungua makipa wa timu nyingine kilimrudia kwenye mchezo dhidi ya Simba SC, uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita katika Uwanja wa Majaliwa, mjini Ruangwa mkoani Lindi.

Sey ametoa kauli hiyo kufuatia aina ya ushangiliaji alioutimia mghana mwezake Bernard Morrison, baada ya kuifungia Simba SC bao la tatu na la ushindi katika mchezo huo.

Sey ambaye ni rafki mkubwa wa Morrison amesema kitendo cha kiungo huyo kushangilia mbele yake, baada ya kufunga bao kwa kumtungua mlinda mlango wa Namungo FC Jonathan Nahimana, kimempa fundisho na ndio maana aliamua kutumia msemo wa Kiingereza usemao, “What goes around comes around,”

Sey pia akazungumzia mustakabali wa Namungo FC, baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Simba SC kwa kusema: “Bado safari inaendelea na hizi ni mbio ndefu, tulikuwa kwenye nafasi ya kuushinda mchezo lakini mambo yaligeuka na tukajikuta tukipoteza, nadhani uzoefu umewabeba Simba,” amesema.

Sey alimsifu rafikiye huyo wa karibu Morrison kwa bao lile akisema ni moja ya mabao bora kabisa.

Mchezaji mwingine wa Namungo, beki Steven Duah, Sey na wachezaji wengine wengi raia wa Ghana waliopo nchini wakiwamo wanaocheza katika ligi za chini hutembelea nyumbani kwa Morrison na wamekuwa wakisaidiana katika mambo mbalimbali na wamekuwa pia wakiongea kwa simu na kutambiana kirafiki kabla na baada ya mechi zao.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Juni 2, 2021
Waziri Ummy atangaza waliochaguliwa kujiunga kidato cha tano, vyuo 2021