Soka la nchini Brazil, limepata pigo kubwa baada ya kumpoteza shabiki maarufu wa timu yao ya taifa  ambayo inasifika duniani kwa kuongoza kwenye orodha ya timu zilizotwaa ubingwa wa dunia mara nyingi.

Shabiki, Clovis Fernandes, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 60 na taarifa za msiba zilithibitishwa na watu wa karibu wa mzee huyo ambaye siku zote aliifuata timu ya taifa lake popote pale duniani.

Fernandes, aliyekua anajulikana kwa jina la utani la ‘Gaucho da Copa’, alianza kuonekana katika viwanja mbalimbali vya soka kwa kuifuatilia timu ya taifa ya Brazil kuanzia mwaka 1990 katika fainali za kombe la dunia ambazo zilichezwa nchini Italia.

Shabiki huyu nguli mara zote alikua anaamini kombe la dunia ni halali kwa nchi yake, na alithibitisha hatua hiyo kwa kubeba mfano wa kombe hilo wakati wote wa fainali za kombe la dunia za miaka yote aliyoonekana uwanjani.

Fernandes, alikua mmoja wa mashabiki walioangua kilio wakati timu ya taifa ya Brazil ilipobondwa kichapo cha paka mwizi cha mabao 7-1, katika mchezo wa hatua ya nusu fainali wa michuano ya kombe la dunia dhidi ya Ujerumani mwaka 2014.

Takwimu zinaonyesha kwamba Gaucho da Copa, aliwahi kuhudhuria michezo 154 iliyoihusu timu yake ya taifa, na amesafiri katika nchi 66 duniani kote.

Arsenal Wafuata Madudu Ya Man City, Man Utd
Lowassa Aiteka Chato Kwa Magufuli, Picha Sita