Aliyekua Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ Shaffih Dauda amempinga Rais wa Shirikisho hilo Wallace Karia kuhusu hoja ya Michuano ya Soka la Mtaani ‘Ndondo’.
Mwanzoni mwa juma hili Rais Karia alisema Ligi za Dar es salaam zimekosa msisimko kwa sababu ya Michuano ya Ndondo, kauli ambayo iliibua mijada mbalimbali kwa wadau wa soka nchini.
Akiwa katika Kipindi cha Sports Extra cha Clouds FM jana Ijumaa (Machi 04) Shaffih alisema: “Mashindano yanayofanyika ya mitaani ni mashindano ambayo yamekuwepo miaka nenda rudi, naamini hata hata Rais Karia atakuwa amecheza kwa namna moja au nyingine siku moja kwenye makundi huko Tanga nyumbani alikokulia, kwa hiyo ni utamaduni ambao upo na sidhani kama unaweza kuzuiliwa na mtu yeyote kwamba mpira usichezwe.
“Na kama ikitokea hivyo itakuwa jambo la ajabu kwa sababu dunia nzima inapambana kupromoti mpira wa miguu uchezwe kwa namna yoyote ile, kwa nchi kama Tanzania sidhani kama hilo jambo linaweza likatokea kwa maana sasa badala ya ku-encourage na kutengeneza mifumo mizuri ya kuwapa nafasi vijana kucheza eti uje na wazo la kuzuia mashindano yasifanyike.”
Nimesikia alichokuwa anazungumza Rais Karia, kwanza sijaona sehemu aliyozuia mashindano kufanyika, alikuwa na concern yake ya mashindano ya kufanyika kipindi cha msimu, akihisi kwamba yakifanyika wakati wa msimu wakati mashindano yanaendelea inaweza ikaleta mkanganyiko”
Kauli ya Karia iliyoibua mijadala ya wadau wa soka kuhusu Michuano ya soka la Mtaani ‘Ndondo’: “Ligi za Dar zimekosa msisimko kwa sababu ya Ndondo. Chama cha soka Dar kimeruhusu Ndondo kuchezwa wakati ligi ya mkoa inaendelea. Lakini pia ndondo zinatuumizia sana wachezaji wa ligi kuu. Nataka tuwe wakali sasa na Ndondo”
Februari 16, Kamati ya maadili ya TFF ilimfungia Shaffih Dauda alifungiwa kuji kujihusisha na soka kwa kipindi cha miaka mitano na kutozwa faini ya shilingi milioni sita (6,000,000).
Shaffih alituhumiwa kuchapisha taarifa ya uongo kwenye ukurasa wake wa Instagram dhidi ya Shirikisho hilo, ambazo zilidaiwa kuwa na uchochezi.
Shaffih alifanya kosa hilo ambalo linakwenda kinyume na vifungu vya 73 (4)(a) pamoja na 75(5) vya kanuni za maadili za Shirikisho hilo, Toleo la 2021. Pia kwa kukiuka kifungu cha 3(1) cha kanuni za utii za TFF, Toleo la 2021.