Mwanahabari Shaffih Dauda aambaye alitangaza kujitoa katika mchakato wa kuwania nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), amerejea kwenye mchakato huo.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Dauda ametangaza kurejea katika kugombea nafasi hiyo kwenye Uchaguzi Mkuu wa TFF unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, 2017 mkoani Dodoma baada ya kukata rufaa ambayo ilisikilizwa kisha kufutwa kwa tuhuma zilizodai kuanza kampeni mapema.
Katika ukurasa wake huo, Dauda ameandika haya:
Hatua ya Kwanza:
Nilijitoa kwenye uchaguzi kutokana na siasa za soka ambazo mimi siyo muumini wake na sikupenda kuhusishwa nazo. Baada ya tamko langu viongozi wangu kwenye nyanja mbalimbali za ndani na nje ya soka, walinifuata na kuniuliza sababu za kufanya hivyo na kunishawishi nirudi kwenye uchaguzi. Lakini mimi binafsi nikaamua kuendelea na maamuzi yangu.
Hatua Ya Pili:
Nilitangazwa kuondolewa kwenye uchaguzi kwa kujihusisha na vitendo visivyokubalika kwenye uchaguzi, ikiwemo kuanza kampeni mapema. Kwa sababu haikuwa kweli na mimi binafsi sikupendezwa na jinsi jina langu lilivyochafuliwa. Nikaamua kukata rufaa ili nisafishwe na kutoka kwenye tuhuma hizo. Nashukuru kamati ya rufaa imekubali rufaa yangu tuhuma za kuanza kampeni mapema na mengine hazipo tena juu yangu.
Hatua Ya Tatu:
Kwa ruhusa yenu wadau, wakubwa wangu na wadogo zangu mlionishawishi niendelee na mchakato. Narudi tena kwenye mchakato baada ya kusafishwa juu ya tuhuma zilizotolewa. Nimefarijika kuona viongozi wa mpira hadi wa serikali walivyoumia baada ya mimi kujitoa kwenye mchakato. Hivyo basi kwa uzalendo wa soka la bongo, tutaendelea kupambana kunyoosha kila kilichopinda ili soka la bongo liwe kwenye mstari.