Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Shafih Dauda amefungiwa kujihusisha na soka kwa kipindi cha miaka mitano na kutozwa faini ya shilingi milioni sita (6,000,000).
Shaffih amekumbwa na adhabu hiyo baada ya kukiri mbele ya kamati ya maadili ya TFF kuchapisha taarifa ya uongo kwenye ukurasa wake wa Instagram dhidi ya Shirikisho hilo, ambazo zimedaiwa kuwa na uchochezi.
Taarifa iliyotolewa na TFF kupitia kurasa zake za Mitandao ya kijamii leo Jumatano (Februari 16), imeeleza kuwa, Shaffih alifanya kosa hilo ambalo linakwenda kinyume na vifungu vya 73 (4)(a) pamoja na 75(5) vya kanuni za maadili za Shirikisho hilo, Toleo la 2021. Pia kwa kukiuka kifungu cha 3(1) cha kanuni za utii za TFF, Toleo la 2021.
Mwingine aliyehukumiwa na Kamati ya Maadili ya TFF ni Hawaiju Gantala kwa kosa la kupeleka masuala ya mpira wa miguu katika Mahakama za kawaida.
Gantala amefungiwa Maisha kujihusisha na masuala ya Soka ndani na nje ya Tanzania.