Aliyekua Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la soka nchini Tanzania ‘TFF’ Shaffih Dauda amethibitisha kupokea taarifa ya kufungiwa kujihusisha na Soka kwa kipindi cha miaka mitano na kutozwa faini ya Shilingi Milioni Sita (6,000,000).
Jana Jumatano (Februari 16), TFF kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ilitoa taarifa ya kufungiwa kwa Shaffih Dauda, baada ya Kamati ya Maadili ya Shirikisho hilo kumkuta na hatia ya kutoa taarifa za Uongozi kupitia Ukurasa wake wa Instagram mapema mwezi huu Februari.
Shaffih Amesema: “Nimepokea taarifa kama ilivyotangazwa. Naiendesha akaunti kama Taasisi inayofanya kazi na watu wengi. Nimejaribu kuwaambia jinsi ninavyofanya kazi.”
“Binafsi sina shida na yeyote. Sioni kama kuna nililopoteza. Sasa narudi kufanya kazi za Uandishi wa Habari. Kwanza nitakuwa huru kama Mwanahabari.”
“Nitaendelea kufanya kazi zangu maana leseni yangu ya Maudhui imetoka TCRA. Wao (TFF) watani’contor katika masuala ya kiuongozi, lakini sio masuala yangu mengine binafsi”
Kamati ya Maadili ya TFF pia imemfungia Maisha kujihusisha na soka ndani na nje ya Tanzania, aliyekua Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Biashara United Mara Hawaiju Gantala kwa kosa la kupeleka masuala ya mpira wa miguu katika Mahakama za kawaida.