Maamuzi ya michezo ya Ligi Kuu kuchezwa jijini Dar es salaam, yamepokelewa tofauti na mkuu wa idara ya habari na mawasiliano ya Mbeya City FC Shaa Mjanja.

Maamuzi hayo yalitangazwa juma lililopita na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Harrison Mwakyembe alipozungumza na waandishi wa habari mijini Dodoma, siku moja baada ya Rais Magufuli kuruhusu michezo iendelee kuanzia Juni Mosi.

Mjanja amesema maamuzi ya michezo yote ya ligi ichezwe mkoa mmoja sawa na michezo hiyo kuchezwa ugenini, huku klabu shiriki zikiumizwa na gharama za kambi.

“Viwanja vya mazoezi, chakula na mambo mengine ambayo ni vyema kufanyiwa tathimini kabla ya kurejesha ligi kwamba vilabu vinawezeshwaje?” aliohoji Mjanja.

Katika hatua nyingine Mjanja amesema klabu yao ni sehemu ya klabu zilizoyumba kiuchumi kutokana na janga la maambukizi ya Corona, hivyo wamejipanga kuweka kambi jijini Mbeya na si Dar es salaam, kuepuka gharama.

“Suala la kuweka kambi Dar es salaam lina changamoto kubwa sana, hali ya kiuchumi haipo sawa.”

Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Young Africans ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.

Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.

Na katika ASFC timu zilizofanikiwa kutinga Robo Fainali ni Alliance FC ya Mwanza, Namungo FC ya Ruangwa, Lindi, Ndanda FC ya Mtwara, Kagera Sugar ya Bukoba, Azam FC, Simba SC, Young Africans za Dar es Salaam na Sahare All Stars ya Tanga, timu pekee ya Daraja la Kwanza.

Ianis Hagi kubaki Ibrox Stadium
Serikali yatoa sababu kuchelewa uzalishaji sukari kiwanda cha Mkulazi