Shahidi wa tisa Mary Mayoka (40) ambaye ni Meneja wa benki ya CRDB tawi la Kwa Mrombo, jijini Arusha, katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya (34) na wenzake sita, amedai aliidhinisha mfanyabiashara, Francis Mroso atoe Sh milioni 90 kwa mkupuo.
Akiongozwa na Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Serikali, Tasilia Asenga, shahidi huyo amesema alimhoji mfanyabiashara huyo kwa nini alitaka kutoa fedha hizo kwa wakati mmoja na alimjibu kuwa alitaka kumlipa mtu aliyefuatana naye benki hapo.
“Nilimfuata yule kijana (mlipwaji) kuzungumza naye kumuuliza kama ana akaunti benki na alinijibu kwamba hana na nilimshauri afungue akaunti lakini alikataa alitaka kulipwa fedha taslimu na alisema angekuja siku nyingine kufungua akaunti,” alidai shahidi huyo.
Shahidi huyo alidai kwamba Januari 22, mwaka huu, saa 11 jioni, alifika ofisini kwa Mhasibu wa benki ya CRDB kumweleza kuwa Mroso anataka kutoa fedha nyingi hivyo alitaka kwenda kuzungumza naye kama meneja wa tawi hilo.
Sabaya na wenzake wanakabiliwa na mashitaka matano likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji wa fedha, kujihusisha na vitendo vya rushwa, kuongoza genge la uhalifu na kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Silvester Nyengu (26), Enock Togolani (41), Watson Mwahomange (27), John Odemba, Jackson Macha(29) na Nathan Msuya (31).