Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amelaani shambulio lilitokea nchini Afghanistan, ambalo limesababisha vifo vya raia takribani 19 na wengine kujeruhiwa.
Taarifa iliyotolewa jijini New York, Marekani na Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq imesema shambulio hilo limetokea katika uwanja wa Kimataifa wa mchezo wa kriketi, kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.
Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha na kutaka ahueni ya haraka kwa majeruhi, huku akisisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya raia ni kinyume cha sheria za kimataifa za kibinadamu.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, mlipuko huo ulitokea wakati mchezo ukiendelea katika siku hii ya Ijumaa Julai 29, 2022 ambayo huwa ni siku ya mapumziko Afghanistani.
Naye, Naibu Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan, Dkt. Ramiz Alakbarov ambaye alikuwa uwanjani akishuhudia mechi hiyo, amelaani shambulio hilo akisema ni la kikatili.
Dkt. Alakbarov ambaye pia ni Naibu Mkuu wa ujumbe wa Umoa wa Mataifa nchini Afghanistan (UNAMA) alikwepo uwanjani hapo kuhutubia chama cha Kitaifa cha kriketi nchini humo na ametuma salamu za rambirambi kwa wafiwa na kuwatakia majeruhi ahueni ya haraka.
Taarifa iliyotolewa na UNAMA mjini Kabul, imemnukuu Naibu Mkuu wa ujumbe wa Umoa wa Mataifa nchini Afghanistan, akitaka uchunguzi ufanyike na wahusika wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.