Shehena ya pombe kali zilizofungwa katika vifungashio vya plastiki  (Viroba) zenye thamani ya shilingi bilioni 2 zimekamatwa Jijini Dar es Salaam katika operesheni inayoendelea ya kuondoa pombe hizo nchini.

Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Manchale Heche ameyasema hayo leo, Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na vyombo vya habari katika operesheni hiyo ambayo inaendelea kwa nchi nzima.

“Bado tunaendelea na operesheni ya ukamataji na uzuiaji wa pombe za viroba, ambapo leo katika ghala la kampuni ya Lovekira iliyoko Tegeta, Wazo tumefanikiwa kukamata zaidi ya katoni 7000 za pombe za viroba aina ya Konyagi, Valeur, Burudani na Zanzi ambazo ujazo wake ni kati ya mililita 50 mpaka 200,” amesema Heche.

Aidha, amesema kuwa, licha ya shehena ya viroba iliyokutwa katika ghala hilo bado kampuni hiyo inaendelea kuingiza mizigo ya viroba ambapo timu iliyofika kukagua ghala hilo ilikuta katoni nyingine za pombe hizo zikiwa ndani ya gari zikisubiri kuingizwa ndani ya ghala hilo.

Kwa upande wake Meneja wa kampuni hiyo, Siah Mboya amesema kwamba viroba vilivyokuwa ndani ya gari vilikuwa vikihamishwa kutoka tawi lingine la kampuni hiyo lililoko Tegeta kutokana na Serikali kusitisha uuzaji na usambazaji wa pombe hizo.

Nae, Afisa Afya wa Manispaa ya Kinondoni John Kijumbe amesema kwamba, baada ya kutambua idadi ya pombe za viroba iliyokamatwa. Muhusika wa mzigo uliokamatwa pamoja na Afisa wa Serikali husaini fomu inayotaja kiasi cha pombe kilichokamatwa na kupewa maelekezo ya kutoondoa mzigo huo mpaka Serikali itakapotoa maelekezo.

Operesheni ya kuondoa pombe za viroba ni utekelezaji wa tamko la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kusitisha uzalishaji, usambazaji, uuzaji na matumizi ya pombe hizo kuanzia Machi 01, 2017.

 

Lionel Messi ategua mtego, wataalam wamsaidia
Ndalichako atoa maagizo bodi mpya ya VETA