Aliyekuwa Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam, Alhad Mussa Salum ambaye uteuzi wake ulitenguliwa kuanzia Februari 02, 2023, amesema amepokea uamuzi huo kwa mikono miwili na kudai uongozi ndivyo ulivyo na hupangwa au kuondolewa kwa nyakati sahihi.
Sheikh Alhad Mussa Salum ameyasema hayo hii leo Februari 3, 2023 wakati akizungumza kwa njia ya simu na Dar24 Media na kuongeza kuwa hana kinyongo na kilichotokea kwakua mamlaka zimeona ni sahihi kufanya hivyo kutokana na mahitaji husika.
Alipoulizwa kuhusu kuondolewa kwake na sintofahamu ya sakata la talaka ya Dkt. Mwaka na mkewe, Sheikh Alhad amesema hana la kuzungumza kuhusiana na tukio hilo na kwamba anachoangalia kwa sasa ni majukumu yake yaliyo mbele.
Baraza la Ulamaa likiongozwa na Mwenyekiti wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally lilitengua uteuzi wa Sheikh Alhad Mussa Salum wa Mkoa wa Dar es salaam baada ya kufanyika kwa kikao chake Jumatano February 1-2, 2023 Jijini Dar es Salaam.
Kufuatia utenguzi huo, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally amemteua Sheikh Walid Alhad Omar, kukaimu nafasi ya Sheikh wa Mkoa wa Dares Salaam kuanzia February 02, 2023.