Kiongozi wa Kiislamu Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Sheikh Ali Amini ameuawa kwa kupigwa risasi wakati akisali swala ya Magharibi kwenye Msikiti Mkuu Mjini Beni.

Mwanaharakati Mjini Beni Stewart Muhindo amesema kuwa Kifo cha Sheikh Amini wakati huu wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani umesababisha mshtuko mkubwa mjini Beni, mji ulio na watu karibu 200,000.

”Ilitokea wakati wa swala ya Magharibi. Risasi zilifyatuliwa ndani ya msikiti na kumpata Imam. Mtu huyo alitoka eneo la tukio, alikuwa na mwenzake ambaye alikuwa akimsubiri na pikipiki”. Muhindo ameiambia BBC.

Hata hivyo Shirika la habari la Reuters limesema kuwa Kiongozi huyo alikuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya wanamgambo wa kiislamu kwenye eneo hilo.

Mashariki mwa Congo imekumbwa na hali mbaya ya usalama, ikiwemo mashambulizi yanayodaiwa kutekelezwa na kundi la wanamgambo wa Kiislamu (IS).

IS imedaiwa kutekeleza mashambulio kadhaa ya Allied Democratic Forces (ADF), lakini haijulikani makundi haya mawili yana uhusiano wenye nguvu kiasi gani.

Kundi hilo limeongeza mashambulizi dhidi ya raia tangu DRC ilipoanza vita dhidi ya kundi hilo mwezi Oktoba mwaka 2019. Karibu watu 200 wameuawa na kundi la ADF tangu mwezi Januari. Umoja wa Mataifa umeeleza.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Mei 9, 2021
Serikali yamzawadia Mercedez Benz Mzee mwinyi