Serikali imepanga kutunga sheria itakayowabana watu wasiowatunza wazazi wao wanapofikia katika hali ya uzee.
Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Naftali Ng’oli ameweka wazi mpango huo wa Serikali jana jijini Dodoma, alipokuwa akifungua maadhimisho ya siku ya kuelimisha na kupinga ukatili kwa wazee.
Amesema kuwa mpango huo umewekwa mezani kwa kuzingatia namna ambavyo wazazi wamekuwa wahangaika kuwalea watoto wao na hata kuchukuliwa hatua kisheria pale wanaposhindwa kutekeleza jukumu hilo kwa ukamilifu, lakini wanapokuwa wakubwa huwaachana wazazi wao wakihangaika bila kuchukuliwa hatua.
“Vijana wamekuwa wakiwatelekeza wazazi wao pindi wanapofikia hali ya uzee na kutokana na hali hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine inatunga sheria itayowabana,” Kamishna Ng’ondi anakaririwa.
Aliongeza kuwa tayari kuna baadhi ya nchi ambazo sheria hiyo imeshaanza kufanya kazi na vijana wenye tabia hiyo wamekuwa wakichukuliwa hatua.
Aidha, alisema kuwa Serikali inaendelea kufanya mpango wa kutoa pensheni kwa wazee kwani walifanya kazi kwa bidii walipokuwa vijana kulitumikia taifa, hivyo hakuna budi kuwapa pensheni wanapoishiwa nguvu.
Alisema kuwa kama upande wa Zanzibar tayari wameaza kutekeleza mpango huo wa pensheni kwa wazee, upande wa Bara pia watakamilisha taratibu na kuanza kufanya hivyo kwani hakuepukiki.