Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania – TAMWA – ZNZ, Dkt. Mzuri Issa amesema ni muhimu kuwa na sheria nzuri za Habari ambazo zitapelekea uwepo kwa uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza kwa jamii.
Mzuri ameyasema hayo katika Mkutano wa kutoa mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya tume ya utangazaji ya Zanzibar (No. 7, 1997), uliowashirikisha Kamati ya masuala ya Habari – ZAMECO, asasi za kiraia na tume ya kurekebisha ya sheria uliofanyika Mazizini Zanzibar.
Amesema, “Uhuru wa Habari na haki ya kupata habari pamoja na uhuru wa kujieleza ni mambo ya msingi katika maendeleo ya nchi na inaleta hata furaha ya mtu binafsi.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa tume ya kurekebisha Sheria Zanzibar, Khadija Shamte amesema wakati umefika wa na sheria zinazokwenda na wakati na tume iko tayari kushirikiana na wadau kwenye kupokea maoni ya kurekebisha sheria, ili kutoa fursa za kiushindani wa utoaji taarifa kwa vyombo vya Habari.