Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amewataka wamiliki wa vyombo vya habari na waandishi wa habari kuhakikisha wanajipanga ili kuendana na matakwa ya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari (2016), itakayoanza kutumika Januari 2022.
Akizungumza na wahariri pamoja na waandishi wa habari, Jijini Dar es Salaam, Bashungwa amesema sheria hiyo itakapoanza kutumika changamoto nyingi zitakwisha.
“Niwaambie tu Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 ambayo imetoa muda mrefu kwa media (vyombo vya habari) na waandishi kujiandaa ambao unaisha Desemba mwaka huu, tutaanza kuitumia rasmi Januari mwaka 2022, hivyo kama kuna ambao hawajakidhi matakwa ya sheria hiyo wahakikishe kabla ya Januari hiyo wanakuwa na vigezo,’’ amesema Bashungwa.
Bashungwa amesema kuwa kwa upande wa waandishi wa habari ili kufanya kazi ya uandishi wa habari sheria hiyo inawataka kuwa na sifa ya elimu angalau kuanzia ngazi ya stashahada kutoka vyuo vinavyotambulika.