Serikali imeanza kutekeleza Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi ya mwaka 2016 (The Whistleblower and Witness Protection Act. 2016) ili kuimarisha utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu nchini.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Kamana Stanley wakati akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo jijini Dar es Salaam kuhusu kuanza kutumika kwa sheria hiyo.

Stanley amesema kuwa  kuwepo kwa sheria hiyo kutasaidia kuwapatia ulinzi wa kisheria wale wote wanaotoa taarifa za uhalifu wa makosa ya aina mbalimbali wanayoshuhudia yakitendeka. Taarifa hizo zitatolewa na kupokelewa sio tu kwenye vyombo vya dola pekee bali pia kupitia vyombo vya habari na vyanzo vingine vinavyobainishwa katika sheria hiyo.

“Wananchi wasiwe na woga kujitokeza kutoa taarifa za uhalifu na matendo ya aina zote yanayofanywa kinyume cha sheria kwani taarifa hizo zitakuwa siri na zitafanyiwa kazi bila ya kuwataja watoa taarifa. Pia mashahidi wanapotakiwa kufika mahakamani wasiogope kwani sheria hii inawalinda” alisema Stanley.

Aidha, Stanley ameeleza kuwa katika sheria hiyo wale ambao taarifa zao zitafanikisha kuokoa mali ya umma, kupatikana kwa wahalifu na kulinda mazingira na maisha ya binadamu kutokana na uhalifu uliopangwa kufanyika, wamewekewa utaratibu wa kupatiwa motisha ikiwa ni pamoja na kuwafidia wale ambao wataathirika kutokana na taarifa walizotoa.

“Masuala ya usimamizi wa utawala wa sheria yataimarika kutokana na kuwepo kwa utayari wa wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya uhalifu kwa kufika katika vyombo vya sheria kutoa ushahidi. Pia ushiriki wao katika kufichua maovu yakiwemo yanayosababisha hasara kwa taifa utasaidia kuinua uchumi ukizingatia kwamba sasa hivi Serikali inapambana sana na mafisadi” alisema Stanley.

Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi ya mwaka 2016 (The Whistleblower and Witness Protection Act. 2016)imeanza rasmi kutumika Julai Mosi mwaka huu baada ya kuidhinishwa na Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe

Aishi Manula: Ninashukuru Kwa Pongezi Za Nyota Wa Nigeria
Wizara Ya Habari, Utamaduni, Sanaa Na Michezo Kuunda Sera Mpya Ya Sanaa