Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Dkt. Gerald Ndika amewataka Majaji na Mahakimu kutafsiri sheria zinaohusu masuala ya wanawake na watoto ili ziendane na mazingira ya sasa katika kuendesha mashauri yanayohusu masuala la unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.
Akizunguza wakati wa mafunzo ya haki za binadamu na unyanyasaji hususani kwa wanawake na watoto, yanayofanyika Mjini Bagamoyo Mkoa wa Pwani Jaji Ndika alisema kuwa sheria zilizopo kwa kiwago kikubwa zinajitosheleza kinachotakiwa jinsi ya kuzitafasiri, hivyo Majaji na Mahakimu watoe tafsiri ambayo inaendana na mazingira ya matukio yalivyo.
Jaji Ndika ambaye ni mshiriki katika mafunzo hayo, amesema kuwa moja ya faida zake ni kuwaandaa wawezeshaji katika eneo hilo ili kusaidia Mahakama ya Tanzania, Majaji wa Mahakama ya Rufani,Majaji wa Mahakama Kuu, Mahakimu,watumishi mbalimbali ambao wanatoa maamuzi juu ya vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa wanawake na watoto kuwa na umahiri.
‘‘Matukio haya yanatokana na mambo mengi ikiwemo mila potofu pamoja na uelewa wao mdogo, wanaona kumpiga mke au mtoto ni jambo la kawaida na ana haki ya kufanya hivyo. Lakini ubora wa mafunzo haya yatasaidia kupata wakufunzi ambao wataenda kuwapa wengine elimu juu ya kuweza kupambana na ukatili na unyanyasaji wa wanawake na watoto,’’ amesisitiza Jaji Ndika.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Joaquine De Mello akifungua rasmi mafunzo hayo, amesema kuwa yana lengo la kuwawezesha watoa maamuzi kuwa na uweledi zaidi wa kutoa haki na pia kuielimisha jamii juu ya haki zao za msingi na tatizo la unyanyasaji na ukatili wa kijinsia ambalo limekithiri.
Ameongeza kwamba kumekuwa taarifa nyingi zinazotolewa na vyombo vya habari pamoja na wanajamii ambao wamejitokeza wazi kutoa matukio mbalimbali juu ya suala hilo. Pia tafiti mbalimbali ambazo zimefanywa hivyo wamegundua kuwa matukio mengi ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia yanafanywa wahusika wanaotuhumiwa kuwa ni familia au ndugu wa karibu.
Mshiriki mwingine wa mafunzo hayo, ambaye Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine,iliyopo Jijini Dar es Salaam, Hanifa Mwingira alisema jamii inapaswa kuona kuwa vitendo hivyo ni vibaya na kila mtu anapaswa kusema ‘ukatili sasa basi na mtoto wa mwenzako kuwa ni mtoto wako na hupaswi kumfanyia ukatili,’.
Jumla ya washiriki 26 wanapatiwa mafunzo juu ya masuala ya unyanyasaji na ukatili kijinsi. Mafunzo hayo yameanza Juni 27, mwaka huu na yatamalizika Julai Mosi, mwaka huu.