Kiungo Mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Miraji Athumani ‘Sheva’, ameelezea furaha yake ya kurejea tena Ligi Kuu akiwa na timu yake mpya ya JKT Tanzania, kwa kuwa alikuwa akitamani kuchezaji ligi moja na straika wa Yanga, Fiston Mayele na winga wa Simba, Pape Sakho.

Miraji ambaye aliichezea Klabu ya Simba SC mwaka 2019 hadi 2020, amesema ni bahati iliyoje kurejea tena kwenye Ligi Kuu na kwamba ndoto yake ilikuwa kuwa ligi moja na baadhi ya mastaa anaowakubali kwa sasa, Mayele na Sakho.

“Nawakubali wengi, lakini hawa wachezaji wanacheza kwenye nafasi ambayo mimi nacheza na naiga vitu vingi kutoka kwao, mimi ni straika na winga pia, Mayele yeye kosa moja goli moja, Sakho ni msumbufu, mimi pia kuna viti naokota huko, sasa na mimi nimekuja huko huko, nitaonyesha nilichokuwa nacho, kikubwa tu ni kumuomba Mungu nisipate majeraha,” amesema Miraji ambaye mashabiki wake wanamwita ‘Sheva’, wakimfananisha na Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, AC Milan na timu mbalimbali za barani Ulaya, Andriy  Shevchenko.

Akiwa ni mmoja wa wachezaji walioipandisha daraja JKT Tanzania kutoka Ligi ya Championship msimu huu, amethibitisha kubaki kwenye kikosi hicho kwa sababu hajapokea ofa yoyote kutoka timu zingine.

“Safari ya Championship ilikuwa ndefu na ngumu, nilimisi kucheza Ligi Kuu na timu kubwa, timu nzuri ili nionyeshe tena nilichokuwa nacho kwa sababu mashabiki wengi hawajaniona na wamenisahau kwani muda mrefu sikucheza soka kutokana na kuwa majeruhi.

“Nilipata majeraha, nilivunjika mfupa mdogo wa mguu wa kushoto, ndicho kilichosababisha kupotea kwa muda mrefu kwenye ramani ya soka, sasa nimepona, maisha yanaendelea nipo  JKT Tanzania si Simba tena,” amesema

Wakati huo huo, timu ya JKT Tanzania juzi Jumatatu (Mei 15) ilikabidhiwa kombe lao la ubingwa wa Championship kwenye mechi maalum iliyochezwa Uwanja wa Uhuru dhidi ya Transit Camp na kutoka sare ya mabao 2-2.

SMZ kuboresha ligi za soka Zanzibar
Marcel Sabitzer ndio basi tena Man Utd