Mchezani wa zamani wa klabu za Simba, Coastal Union, JKT Tanzania na Dodoma Jiji, Ally Ahmed Shiboli amesema kwa sasa yupo huru baada ya ugonjwa wa Corona kukwamisha dili lake nchini Kenya.
Shiboli ambaye aliwahi kuitumikia timu ya taifa ya Zanzibar *Zanzibar Heroes*, amesema alikua kwenye mipango ya kucheza soka nje ya nchi (Kenya) lakini janga la maambukizi ya Corona lilikwamisha mipango yake, licha ya klabu kadhaa nchini humo kuonyesha nia ya kumsajili.
“Baada ya kumaliza mkataba wangu Tanzania nilielekea Kenya lakini nikiwa nchini humo nilipata timu tatu (Posta Rangers, Wazito na Chemelil Sugar) zote zikitaka kunisajili lakini likatokea janga la Corona.”
“Kwa hiyo mambo yote yakasitishwa nikarudi nyumbani Tanzania kwa sasa nipo Tanga.” Alisema mshambuliaji huyo.
Hata hivyo Shiboli amesema kwa sasa yupo hapa nchini akifanya mazoezi binafsi, na endapo klabu yoyote itakua tayari kufanya mazungumzo ya kumsajili anaikaribisha.
“Naendelea kufanya mazoezi najiandaa, timu yoyote ikitokea nitasajili kwa sababu mimi ni mchezaji huru sina mkataba na timu yoyote.”
“Timu itakayonihitaji tutaongea. Sichagui timu, iwe Daraja la Pili, Daraja la Kwanza au Ligi Kuu, timu tutakayofikia makubaliano ya maslahi nafanya kazi. Nipo tayari kupambana.” Alisema Shiboli