Wachezaji wa Kigeni Sharraf Shiboub kutoka nchini Sudan na Chekhi Moukoro kutoka Ivory Coast wanadaiwa kutemwa na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, kufuatia kushindwa kumridhisha Kocha Mkuu Franco Pablo Martin kwenye Michuano ya Mapinduzi 2022, itakayofikia tamati leo Alhamis (Januari 13) Kisiwani Unguja-Zanzibar.
Wachezaji hao walicheza kwenye kikosi cha Simba SC kwa lengo la kufanyiwa majaribio ili kupata nafasi ya kusajiliwa katika Dirisha Dogo la Usajili, lakini taarifa zinaeleza kuwa mambo yamewaendea kombo, huku kiungo kutoka nchini Nigeria Udoh Etop David akikidhi vigezo vya Kocha Pablo.
Kiungo huyo alitua nchini Juma lililopita na alipeleka moja kwa moja Kisiwani Unguja-Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, kufanyiwa majaribio.
Udoh akiwa Zanzibar, alifanya mazoezi na timu hiyo huku akicheza mchezo wa kwanza dhidi ya Mlandege FC uliomalizika kwa suluhu na kuonesha kiwango kikubwa.
Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa Simba SC itatoa taarifa za kuthibitishwa kutemwa kwa Sharraf Shiboub kutoka nchini Sudan na Chekhi Moukoro kutoka Ivory Coast na kusajiliwa kwa Udoh baada ya Michuano ya Mapinduzi 2022.
Akizungumzia usajili wa Dirisha Dogo wa Simba SC Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez, amesema: “Kikosi chetu kina wachezaji wengi wazuri jambo la kwanza kuna tuliowaacha ili ipatikane nafasi ya kuingiza wengine kutokana na mapendekezo ya Kocha Pablo.
“Kikubwa Wanasimba wasiwe na hofu, viongozi wao pamoja na makocha wetu tupo makini na tutawasapraizi watu kama tunavyofanya misimu mingine.”
“Kutokana na mkakati tuliokuwa nao viongozi kwa kushirikiana na Kocha Pablo tunahitaji wachezaji waliokuwepo kwenye kiwango bora na kuisaidia timu wakati huu, niwatoe hofu katika usajili huu tutasajili kabla dirisha halijafungwa.”