Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini, John Shibuda amemuomba Rais John Magufuli kuwasamehe wale wanaorejesha fedha walizopewa na Mkurugenzi wa kampuni ya VIP Engendering, James Rugemalira ambazo zimetokana na sakata la Escrow.
Shibuda ameyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku chache baada ya Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja kuwasilisha kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) shilingi milioni 40 alizopewa na Rugemarila.
Alisifu kitendo cha Ngeleja kurejesha fedha hizo akiwataka wengine waliopata gawio la Escrow kuchukua uamuzi kama huo huku akiwaombea msamaha.
“Kwa kitendo chake Ngeleja kutubu, tukubali tusiwe na inda na choyo ila wale wengine nao wakubali kuzirejesha fedha na mheshimiwa Rais awasamehe kama dini zetu zinavyosema, mtu akitubu asamehewe,” alisema Shibuda ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama cha Ada Tadea.
James Rugemalira ambaye pia alikuwa na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL na Mwenyekiti mtendaji wa PAP, Habinder Seth Sigh walifikishwa mahakamani kujibu mashtaka sita ikiwa ni pamoja na uhujumu uchumi.