Msafara wa Katibu Mkuu wa CCM, umesimamishwa maeneo ya Mwela, Mtowisa, Msia, Talanda, Milepa na Kinambo, Milepa akelekea Kioze na Ilemba, ambapo Wananchi wakiwa na ndoo walitaka asikilize kero zao na kutafutia ufumbuzi ikiwemo kero ya uhaba wa maji na namba ya utambulisho wa kijiji chao.
Tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Mwela kilichopo Kata ya Mtowisa, ambapo Chongolo aliwatuliza wananchi hao kwa kutoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Ally kuhakikisha changamoto zao zinatatuliwa ndani ya muda mfupi, ikiwa ni pamoja na kukutana nao kwenye kikao ili wajadiliane namna ya kutatua kero hizo kwa njia shirikishi.
Wananchi hao walimuambia Katibu Mkuu kuwa, “huduma za afya tunazo, umeme tunao, barabara inapitika hata pembejeo za kilimo tunapata. Hatuna tatizo na huduma zingine Katibu Mkuu wa CCM. Changamoto zetu hapa ni mbili tu, maji haya unavyoyaona si salama wala si safi na namba ya kijiji chetu hiki kutotambuliwa huko wilayani.”
Baada ya hali hiyo, pia Chongolo akamuagiza Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, kwa kutumia RUWASA wapeleke gari la kuchimba kisima katika kijiji hicho kwa haraka, wakati wakiendelea kutafuta vyanzo vingine vya uhakika, baada ya Meneja wa RUWASA kutoa taarifa kuwa katika mipango yao kijiji hicho kiko ndani ya maeneo ambayo yamepangiwa mradi wa maji utakaogharimu Tsh. 1.3, utakaokuwa mwarobaini wa kero hiyo.