Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited – GGML, kwa kuendelea kuwa mdhamini mkuu wa maonesho ya sita ya teknolojia ya madini Geita ambayo mwaka huu yanashirikisha zaidi ya washiriki 400.
Akizungumza na Waandishi wa Habari hii leo Septemba 21, 2023 kuhusu maandalizi ya maonesho hayo yanayofanyika katika Viwanja vya Bombambili mjini Geita, Mkuu huyo wa mkoa amesema mwaka jana walishiriki walikuwa zaidi ya 250.
Amesema, Mkoa wa Geita umeweka mazingira mazuri kwa kampuni zinazojihusisha na utafiti wa madini, uchimbaji unaotumia teknoljia rahisi, uchenjua pamoja na uongezaji thamani ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kukua kibiashara.
“Niwakaribishe wawekezaji kuwekeza viwanda vya uchenjuaji pamoja na uongezaji thamani ili kuwaelimisha wachimba wetu kuondokana na matumizi ya kemikali hatari kama vile zebaki. Pia niwakaribishe wananchi wote hasa wanaojihusisha na uongezaji thamani. waje kwa wingi,” amesema.
Maonesho hayo, yatafunguliwa rasmi Septemba 23, 2023 na Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Dotto Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati na yatafungwa na Rais Samia Suluhu Hassan tarehe 30 Septemba 2023.
Meneja Mwandamizi anayesimamia mahusiano jamii – GGML, Gilbert Mworia alisema maonesho hayo yamekuwa na mvuto wa kipekee tangu yalipoasisiwa kutokana na ufadhili wao kupitia mfuko wa uwajibikaji kwa jamii (CSR), ambao uliwezesha ujenzi wa eneo la EPZA na eneo la uwanja huo wa maonesho.
GGML imekuwa kinara wa kuboresha maonesho hayo kwa kuwekeza Sh 800 milioni katika ujenzi wa jengo la utawala la EPZA na msaada wao unavuka usaidizi wa kifedha ambao wameendelea kuutoa kila mwaka.