Klabu ya Schalke 04, inajipanga kumsajili kiungo mshambuliaji kutoka nchini Japan na Leicester City ya England Shinji Okazaki.
Tovuti BILD imeandika, Schalke 04 wapo katika mchakato wa kusaka mshambuliaji atakaewasaidia katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu, na wanaamini Okazaki huenda akawa chaguo sahihi.
Schalke 04 walianzisha mchakato huo, kwa kutumia kigezo cha kumsaka mchezaji ambaye ana uelewa na uzoefu na ligi ya nchini Ujerumani (Bundesliga).
Okazaki aliwahi kucheza soka nchini Ujerumani akiwa na klabu ya VfB Stuttgart na FSV Mainz 05 kabla ya kutimkia nchini England kujiunga na Leicester City.
Hata hivyo mpango wa usajili wa Okazaki umeegemea katika biashara ya mkopo wa muda mfupi, na kama itatokea mchezaji huyo anaondoka atakua amekubali kuachana na hatua ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Leicester City ni miongoni mwa klabu zilizofuzu kucheza hatua ya 16 bora ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, na imepangwa kukutana na Sevilla CF.