Soko kuu la mjini Shinyanga limenusurika kuteketea kwa moto majira ya saa mbili usiku huku chanzo cha moto huo kikiwa kipande cha sigara.
Akisimulia tukio hilo, mwenyekiti wa soko, Alex Stephen amesema moto huo ulianza kuwaka na kuunguza ndoo za plastiki, lakini kutokana na kutokuwa na kasi walinzi na wananchi walifanikiwa kuuzima na kutoleta madhara makubwa.
Akielezea chanzo cha moto huo, amesema inadaiwa mmoja wa watu walioingia kujisaidia kwenye choo cha soko hilo aliitupa kupitia dirishani ikiwa na moto na kuangukia kwenye ndoo ya plastiki, ndipo moto huo ukaanza kuwaka.
“Wakati watu wakiingia kujisaidia chooni walianza kuona moshi ukiingia ndani ya choo kupitia dirishani, ndipo wakatoa taarifa kwa walinzi ambao nao waliomba msaada kwa wananchi waliokuwa karibu na soko hilo, na kuanza kuuzima ambapo walifanikiwa na kutoleta madhara makubwa, zaidi ya kuunguza ndoo” aliongeza.
Kamanda wa Jeshi la zimamoto na uokoaji wilaya ya Shinyanga, Malekela Chimi, amethibitisha kutokea tukio hilo la moto na kubainisha walinzi pamoja na wananchi walifanikiwa kuuzima.
Aidha, amesema wameshatoa maelekezo kwa uongozi wa soko hilo kuondoa bidhaa zote zilizokaribu na choo cha soko pamoja na kutoweka maboksi ambayo nayo yalichochea moto huo kuwaka.