Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameielekeza Wizara ya Maji iendelee kushirikiana na wadau wa sekta ya maji kukamilisha miradi yote inayoendelea kutekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Pia, Waziri Mkuu amesema Wizara ya Maji itengeneze na kutekeleza mwongozo wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) ili kuimarisha uwekezaji katika sekta ya maji kwa kushirikiana na wadau wote muhimu.
Ametoa maelekezo hayo alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye uzinduzi wa Mpango wa Nchi wa WaterAid (2023-2028) na maadhimisho ya miaka 40 ya Shirika la WaterAid Tanzania. Hafla hiyo imefanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Amesema, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua mchango wa Shirika la WaterAid katika kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa awamu zote za utekelezaji wake.
“Kupitia maadhimisho haya, sina budi kuwapongeza Shirika la WaterAid Tanzania kwa kazi nzuri mnayofanya ya kushirikiana na Serikali kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji, usafi wa mazingira na usafi binafsi ambayo imeweza kuleta mafanikio makubwa.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amezitaka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI zitenge fedha za kutosha kuwezesha utekelezaji wa Mwongozo wa Mpango Kabambe wa Afya wa Halmashauri (CCHP). “Hii itasaidia kupatikana kwa huduma muhimu za maji safi na salama, vyoo bora na vifaa vya kunawia mikono zinatekelezwa kwenye vituo vyote vya elimu na afya hapa nchini.”