Baraza la michezo Tanzania (BMT) limefuta uchaguzi wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) na kuvunja uongozi uliokuwepo madarakani huku ikiunda kamati maalum ya watu sita ambayo itafanya kazi kwa muda wa miezi mitatu .
Katibu mkuu wa baraza hilo, Mohamed Kiganja amesema amelazimika kuvunja shirikisho hilo kwa kuwa limekuwa likifanya kazi bila katiba na kusabashisha migogoro ya mara kwa mara ndani ya shirikisho hilo.
Hata hivyo Kiganja ameiagiza kamati hiyo ya watu sita kuhakikisha inarekebisha katiba na kuitisha mkutano mkuu wa uchaguzi na kuratibu shughuli zote ambazo zilitakiwa kufanywa na BFT.
Mwenyekiti mteule wa kamati hiyo Mutha Rwakatare ameihakikishia serikali kuwa atatekeleza vyema maagizo hayo ili kujenga shirikisho imara na lenye tija katika taifa.
Baadhi ya wajumbe walioshiriki katika mkutano huo wametumia nafasi hiyo kuipongeza serikali kwa kuchukua hatua hiyo.
Hivi karibuni BFT imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ya kiutendaji hali ambayo imekuwa ikichangia kuzorotesha mchezo huo.