Kiungo Mshambuliaji Shiza Ramadhan Kichuya amesema yupo tayari kubaki Namungo FC endapo atapata mkataba mzuri na mnono kutoka kwa Uongozi wa klabu hiyo ya mkoani Lindi.
Kichuya alijiunga Namungo FC msimu wa 2020/21 akitokea Simba SC iliyomrejea nchini akitokea Misri alikokua anaitumikia klabu ya Pharco ambayo ilishindwa kumkamilishia maslahi yake binafsi.
Kichuya amesema Uongozi wa Namungo FC una nafasi ya kipekee kumbakisha klabuni hapo, endapo utakuwa tayari kumpatia kile anachokihitaji katika kipindi hiki cha Dirisha la Usajili.
Amesema siku zote anacheza soka kwa maslahi ya kuendesha Maisha yake, hivyo hawezi kuchagua mahala pa kucheza, endapo kila anachokihitaji anakipata kwa wakati kutoka kwa mwajiri wake kwa mujibu wa mkataba.
“Tunacheza soka kwa ajili ya kuendesha maisha yetu, kama watanitimizia ninayohitaji kwa nini niondoke, nitabaki hapa hapa kwa ajili ya kuendelea kufanya kazi yangu ya kucheza soka.” Amesema Kichuya
Kuhusu tetesi za kuhitajika Simba SC Kichuya amesema taarifa hizo anasikia katika baadhi ya vyombo vya habari na kuzisoma kwenye Mitandao ya Kijamii, lakini hakuna lolote ameshathibitishiwa na watu wanaomsimamia kuhusu klabu hiyo ya Msimbazi.
“Sijui, mimi mwenyewe ninazisikia taarifa hizo kama mnavyosikia nyinyi, siwezi kusema sana maana sijui kitakachotokea mbele ya safari, lakini hakuna lolote linaloendelea hadi sasa,”
“Sana, sana huwa ninapokea ujumbe wa simu kutoka kwa mashabiki wa hiyo klabu wananijulia hali na wengine wananiuliza kuhusu uhakika wa kurudi Simba SC, lakini hakuna lolote linaloendelea kwa sasa.”
Shiza Kichuya ni sehemu ya wachezaji watatu waliomaliza msimu wa 2021/22 kwa kufunga mabao matatu kwenye mchezo mmoja ‘Hat Trick’, akiwa sambamba na Jeremiah Juma wa Tanzania Prisons na Idris Ilunga Mbombo wa Azam FC.