Wasanii kutoka Tanzania, Sholo Mwamba na Sarafina wameutambulisha muziki wa Tanzania katika jukwaa jingine la kimataifa walipofanya onesho kwenye ukumbi wa Sea Plaza katikati ya eneo la Dubai Expo.
Wakati watu wa mataifa mbalimbali wakiwa wamesubiria onesho hilo liliilochelewa kuanza kwa sababu za kiufundi, Sarafina ndiye alikuwa wa kwanza kupanda jukwaani na kuimba na kucheza huku akiwashirikisha mashabiki kutoka mataifa mbalimbali kwa kuimba akiwaeleza kisa cha hadithi ya kila wimbo aliouimba.
Safari ya kuitangaza Tanzania ilikolea zaidi alipopanda jukwaani msanii wa Singeli Sholo Mwamba na kuonekana kuwachezesha watu wa mataifa mbalimbali.
“Tumekuja hapa Dubai kutumia sanaa na utamaduni wetu kuitangaza Tanzania. Leo dunia imejua Tanzania kuna singeli na kuna muziki mzuri, usiku huu Sarafina amepata onesho jingine katika ukumbi wa Earth Stage na kazi inaendelea ukumbi mwingine uitwao Sun Stage ambapo Sholo Mwamba na Mrisho Mpoto watafanya shoo nyingine kubwa.
Ni wiki ya sanaa na utamaduni wa Tanzania kwenda “mtaa kwa mtaa” hapa Dubai na “mtaa kwa mtaa” katika kujitangaza duniani,” alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, aliyeshuhudia maonesho hayo Dubai, UAE.