Baada ya kuwa nje ya dimba kwa takribani miezi mitatu, beki wa kulia wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Shomari Kapombe, leo asubuhi ameanza rasmi mazoezi mepesi ya gym.

Kapombe, 23, aliyeichezea Azam FC jumla ya dakika 3188 msimu uliopita, hakufanikiwa kumaliza vema msimu baada ya kuugua ugonjwa wa Pulmonary Embolism (donge la damu kuziba mishipa ya damu katika mapafu).

Beki huyo kisiki mwenye kasi ameanza mazoezi akiwa na furaha kabisa hii inaashiria kuwa yupo fiti kabisa kwa ajili ya kurejea dimbani na kuipigania tena Azam FC msimu ujao, ambapo timu hiyo ina wiki ya pili sasa tokea ianze kujiandaa.

Mtaalamu wa Viungo wa Azam FC, Sergio Perez Soto, ndiye aliyemsimamia programu hiyo aliyoanza nayo, ambapo alimfanyisha mazoezi kadhaa ya kumnyoosha viungo kwa kutumia vifaa mbalimbali vya gym.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz mara baada ya mazoezi hayo, Daktari wa Azam FC, Dr. Juma Mwimbe, alisema kuwa Kapombe ataendelea na programu hiyo mpaka atakapokuwa fiti.

“Tunamshukuru Mungu ameanza mazoezi yake leo, ataendelea na programu ya gym taratibu taratibu hadi wiki ijayo, kama unavyojua hajacheza muda mrefu hivyo tutaendelea kumwangalia zaidi hadi atakapokuwa fiti na baadaye ndiyo tutafanya uamuzi wa kumruhusu kujiunga na wenzake katika mazoezi ya uwanjani,” alisema.

Chanzo: Azam FC

Nay Amesema Amewaachia Wanasheria wake Suala la Basata
Zembwela Akerwa naMabinti Wanaoweka Picha za Utupu Mitandaoni