Mmiliki wa klabu ya Tianjin Quanjian ya China, amethibitisha kufanya mazungumzo na wakala wa mshambuliaji kutoka nchini Hispania na klabu ya Chelsea Diego Costa.
Shu Yuhui ameiambia Tianjin TV kwamba, amezungumza na Jorge Mendes kwa minajili ya kufanikisha biashara ya kumsajili mshambuliaji huyo.
Mwishoni mwa juma lililopita Costa alitemwa kwenye kikosi cha Chelsea kilichopambana na Leicester City baada ya kubwatukiana na meneja wa The Blues Antonio Conte, japo taarifa nyingine zinadai alikua anasumbuliwa na maumivu ya mgongo.
Mmiliki wa klabu ya Tianjin ameamua kujitokeza hadharani na kuzungumzia sakata la usajili wa Costa ambalo kwa siku kadhaa limekua likizungumzwa katika vyombo mbalimbali vya habari duniani kote.
Mbali na mipango ya kutaka kumsajili Costa, pia mmiliki huyo ameweka hadharani mikakati ya kuwawinda wachezaji wengine mashuhuri duniani kama Edinson Cavani, Karim Benzema, Radamel Falcao na Raul Jimenez.
Shu Yuhui
“Mendes alikua nyumbani kwangu siku chache zilizopita na tulizungumza kuhusu suala la usajili wa Costa, na kwa sasa lipo katika mpango mzuri japo litazungumzwa kwa kina siku za usoni,” Alisema Shu.
“Tunaendelea kusubiri na tunaamini hilo jambo linawezekana. Kiukweli tunahitaji mshambuliaji kama Costa na wengine katika klabu yetu, hivyo hatufichi na hatutonyamaza katika mpango huo.”
Klabu ya Tianjin inanolewa na gwiji wa soka kutoka nchini Italia ambaye alikiongoza kikosi cha nchi hiyo kutwaa ubingwa wa dunia katika fainali za mwaka 2006 Fabio Cannavaro.