Imefahamika kuwa Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Moses Phiri hana furaha ndani ya Klabu ya Simba SC, na huenda akaondoka kikosini hapo kama mambo yataendelea kuwa magumnu kwake.
Taarifa kutoka ndani ya Simba SC zinaeleza kuwa Mshambuliaji huyo hana furaha na kuwekwa benchi mara kwa mara na inadaiwa kwa sasa Mzambia huyo ana mipango ya kuondoka endapo ataendelea kusugua benchi.
Phiri ndani ya Simba SC amekuwa na wakati mgumu kutokana na kushindwa kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Msimu uliopita Phiri alianza ligi kuu kwa kasi alifunga mabao 10 na baada ya hapo akakumbwa na majeraha yaliyomfanya awe nje ya uwanja kwa muda mrefu.
Simba SC chini ya benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Robertinho limekuwa likiwatumia zaidi washambuliaji John Bocco sambamba na Jean Baleke tofuati na Phiri ambaye amekuwa akisugua benchi mara kwa mara.
“Phiri hana furaha kabisa kwa sasa ndani ya Simba SC kutokana na kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara, na tayari anafikiria kuondoka kama hali itaendelea kuwa hivi ilivyo.
“Malengo makubwa ya Phiri yalikuwa ni kuisaidia Simba SC katika michuano ya ndani ya kimataifa lakini kote huko amekosa kipaumbele, baada ya kupona alitarajia kuwa angepata nafasi lakini hilo limeshindikana,” kimesema chanzo hicho.
Hata hivyo alipotafutwa Moses Phiri kuzungumzia juu ya suala hilo ambapo alisema hayuko tayari kuzungumzia suala hilo huku akidai kuwa muda utaongea.