Aliyekua mshambuliaji wa klabu za Tottenham Hotspurs na Fulham zote za England, Clint Dempsey ametangaza kustaafu soka, baada ya kucheza katika ngazi ya soka la kulipwa kwa miaka 15.

Dempsey mwenye umri wa miaka 35 amefikia maamuzi hayo, huku akiacha kumbukumbu ya kuwa mchezaji pekee kutoka Marekani aliyefunga mabao mengi zaidi katika ligi ya England.

Tangu alipoanza kucheza soka nchini humo mwaka 2007 akitokea kwenye klabu ya New England Revolution nchini kwao Marekani, mshambuliaji huyo alifunga mabao 50 katika michezo 184 aliyocheza akiwa na klabu ya Fulham mwaka 2007–2012, na alipohamia Tottenham Hotspur mwaka 2012–2013 alifunga mabao 7 katika michezo 29.

Kwa upande wa timu ya taifa ya Marekani, Dempsey pia alifanikiwa kufunga mabao 57 katika michezo 141 aliyocheza tangu mwaka 2004–2017.

“Ilikua ni ndoto yangu kuwa mchezaji wa kimataifa, ninashukuru kukamilisha ndoto hiyo kwa vitendo na mafanikio makubwa,” Imeeleza taarifa iliyotolewa na Dempsey.

“Ninafarijika sana kuwa miongoni mwa wachezaji wa soka wanaotangaza kustaafu kwa heshima kubwa.”

“Sina budi kumshukuru kila mmoja aliyefanikisha safari yangu ya soka, tangu nikiwa na klabu ya New England Revolution kisha Fulham na  Tottenham zote za England, na baadae Seattle Sounders nilipomalizika ndoto yangu ya kusakata soka,”

Image result for clint dempsey retireClint Dempsey

“Daima mchezo wa soka ulinifanya kuhisi nipo nyumbani kila nipokuwa katika majukumu yangu pasina kujali nchi niliyokua nikiishi, nitawakumbuka mashabiki, wachezaji na viongozi wangu kwa kufanikisha ndoto hii.”

Dempsey anaondoka katika medani ya soka huku akiacha kumbukumbu ya kushiriki fainali tatu za kombe la dunia, mwaka 2006 (Ujerumani), 2010 (Afrika Kusini) na 2014 (Brazil).

Ratiba ya ziara za Rais Magufuli mwezi Septemba
Kiba ajiunga na kambi ya Coastal Union