Shule 28 za wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, zikiwemo 11, za msingi na 17, za sekondari zimenufaika na mfumo wa uboreshaji wa miundombinu ya shule wa Lipa Kutokana na Matokeo (EP4R) uliotekelezwa katika kipindi cha tangu 2015 hadi 2020.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa ameyasema hayo jana Septemba 17, 2020 wakati akizungumza na wakazi wa kata ya Nkololo, wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu kwenye mkutano uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Nkololo ‘A’.

Akielezea utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa wakazi hao, Majaliwa amesema awali zilitolewa Shilingi bilioni 2.3 na Septemba mwaka huu zimetolewa Shilingi milioni 457 ili kukamilisha uwekaji miundombinu ya nyumba za walimu, madarasa na matundu ya vyoo katika shule za msingi za Halawa, Kilabela A, Tunge, Mwauchumu, Bukiliguu, Byuna, Chungu cha bawawa, Damidami, Masewa C, Mwashagata na Banemhi zilizoko wilayani humo.

Kuhusu mpango wa elimu bila malipo, Majaliwa amesema shule za msingi 79 zilipatiwa Shilingi Bilioni 3.12 kwa ajili ya ukarabati wa majengo, masuala ya utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu.

Aidha, amesema shule za sekondari 23 zilipatiwa shilingi bilioni 1.43 kwa ajili ya kulipia fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule.

Mpango wa maendeleo wa miaka 10 wazinduliwa
Miili ya watoto 10 yaagwa Bukoba