Waziri wa Elimu wa Kenya, Prof. George Magoha ameagiza shule katika taasisi zote za Elimu ya msingi kufungwa kwa wiki moja kuanzia kesho Agosti 2, 2022 kutokana na Taifa hilo kuwa katika mchakato kujiandaa kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumanne ya Agosti 9, 2022 wiki ijayo.
Hata hivyo, hatua ya Waziri huyo wa Elimu imewashangaza Wazazi na Walimu kutokana na hapo awali shule kuratibiwa kuendelea kwa mapumziko ya nusu muhula wa wiki moja kuanzia Ijumaa iliyopita ya Julai 29, 2022.
“Kama mnavyofahamu, Kenya imepangiwa kufanya uchaguzi wake wa kitaifa Jumanne tarehe 9 Agosti 2022 kwa hiyo kufuatia mashauriano, nawasilisha uamuzi wa Serikali kuhusu kufungwa mara moja kwa taasisi zote za elimu ya msingi kuanzia Jumanne tarehe 2, Agosti 2022,” amesema Prof. Magoha.
Amesema, shule hizo zitakuwa katika mapumziko kupisha uchaguzi hadi siku ya Jumatano Agosti 10, ili kuhakikisha kuwa matayarisho na uendeshaji wa chaguzi zijazo unafanywa kwa urahisi, na kutoa nafasi kwa wapiga kura kushiriki zoezi hilo.