Licha ya kukabiliwa na mchezo wa nusu fainali dhidi ya England kesho jumatano, shirikisho la soka nchini Croatia limetangaza kumtimua kocha msaidizi Ognjen Vukojevic, kufuatia utovu wa nidhamu aliouonyesha kupitia mitandao ya kijamii.
Vukojevic mwenye umri wa miaka 34 ameondolewa kwenye benchi la ufundi la Croatia, kufuatia kuweka video katika mitandao ya kijamii inayounga mkono siasa za Ukaraine ambazo zinakinzana na Urusi.
Pamoja na kumtimua kocha huyo msaidizi, pia uongozi wa shirikisho la soka nchini Croatia limempa onyo beki Domagoj Vida, ambaye ameonekana katika video hiyo akishiriki kutoa maneno yanayounga mkono siasa za Ukraine.
Vida amesamehewa baada ya kuomba radhi kwa kitendo alichokifanya, na uongozi wa shirikisho umemwambia asijaribu kurudia tena utovu huo wa nidhamu ambao huenda ukawachonganisha na nchi ya Urusi, ambayo ina uhusiano mzuri na taifa lao.
Ognjen Vukojevic (Kulia) akiwa na beki Domagoj Vida baada ya mchezo dhidi ya Urusi.
Katika video hiyo, beki huyo anayeitumikia klabu ya Besiktas ya Uturuki ambaye pia aliwahi kucheza nchini Ukraine akiwa na klabu ya Dynamo Kiev, amenekana akisema ‘Glory to Ukraine!’ kabla ya kocha msaidizi Vukejevic kuendelea kusema: ‘Ushindi huu ni kwa ajili ya Dynamo na Ukraine.’
Ognjen Vukojevic pia aliwahi kucheza katika klabu ya Dynamo Kiev mwaka 2008–2015.
Video hiyo ilisambaa katika mitandao ya kijamii, baada ya mchezo wa robo fainali ulioshuhudia Croatia wakiichapa Urusi kwa changamoto ya mikwaju ya penati nne kwa tatu, baada ya timu hizo kwenda sare ya mabao mawili kwa mawili ndani ya dakika 120.