Klabu ya Simba SC imesajili Mlinda Lango kutoka Brazil Jefferson Luis kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Resende ya nchini kwao akitarajiwa kuwa namba moja au mshindani mkubwa wa Aishi Manula atakayekaa nje ya uwanja hadi Novemba mwaka huu baada ya kufanyiwa oparesheni ya nyonga.
Usajili wa Jefferson umezua maswali mengi kwa mashabiki na wadau wengi wa soka nchini kutokana na daraja alilotoka lakini haya ni mambo matano yatakayomfanya acheze Simba SC.
Moja ya vitu ambavyo wadau wamehoji ni pamoja na uwezekano wa Mlinda Lango huyo kupata kibali cha kucheza Bongo licha ya kutoka timu ya kawaida nchini kwao Brazil.
Katika kanuni ya ligi namba 62 inayohusu wachezaji wa kigeni inaeleza; “Mchezaji wa kigeni anayeruhusiwa kusajiliwa kwenye ligi kuu ni yule anayecheza katika timu ya taifa ya nchi yake au Ligi Kuu ya nchi husika.
Mchezaji kutoka Ligi Amerika ya Kusini na Ulaya lazima awe amecheza angalau kuanzia Ligi Daraja la Tatu (Kitaifa kutegemeana na mfumo wa nchi husika).”
Kwa maana hiyo Jefferson atapata vibali vya kucheza nchini kutokana na Brazil kuwepo na mfumo wa ligi kuchezwa kwa majimbo na yeye kutokea Resende timu inayoshiriki Daraja la Kwanza ya jimbo la Rio de Janeiro, ambayo ni miongoni mwa ligi za madaraja matatu ya juu nchini humo.
Pili, Jefferson ametua Simba SC wakati ambao timu hiyo haina Mlinda Lango chaguo la kwanza Manula (mgonjwa) na namba mbili Beno aliyeondoka hivyo kukutana na kipa namba tatu (Ally Salim), na Bwanamdogo Hemed Feruz aliyepandishwa kutoka timu B, hivyo ana nafasi kubwa ya kucheza ndani ya kikosi cha Simba SC mbele ya Ally na Feruz kwani ni pendekezo la Kocha.
Tatu, Baadhi ya mashabiki wa Simba SC na wadau wamekuwa wakihofia Jefferson kushindwa kucheza Tanzania kutokana na mazingira ya soka letu na hali ya hewa sambamba na viwanja. Hata hivyo Bruno Gomes wa Singida United, Gerson Fraga aliyewahi kupita Simba SC na Andre Coutinho aliyepita Young Africans waliweza kucheza vizuri katika hali hiyo hiyo ilihali walitokea Brazil.
Nne, Wadau wanahofia kuhusu lugha ya mawasiliano kwani Watu kutoka Amerika ya Kusini wamekuwa wakizungumza zaidi Lugha zao ikiwemo Kireno, lakini kwa soka la kisasa lugha imekuwa kama nyongeza tu kwani wajuzi wa mambo wanasema ‘Lugha ya Mpira’ ni moja.
Tano ni ushindani dhidi ya Walinda Lango wengine wa Simba SC kwani ambapo baadhi ya wadau wanaamini Manula akipona atarejea kuchukua namba moja yake kikosini jambo ambalo linawezekana au lisiwezekane.
Kocha Mkuu wa Simba Oliveira Roberto ‘Robertinho’ amesema kikosini kwake atakayepata namba ni mchezaji anayejituma na kufanya vizuri na si mazoea.