Watu 123 wameteketea kwa moto katika jiji la Ahmedpur Mashariki nchini Pakistan baada ya roli lililokuwa limebeba mafuta kushika moto.
Kituo cha runinga cha Geo cha Pakistan kimeripoti kuwa chanzo cha moto huo kinasadikika kuwa ni mtu aliyekuwa anavuta sigara katika eneo la tukio, akiwa karibu na roli hilo lenye mzigo wa mafuta ambalo linadaiwa kupinduka kabla ya kushika moto.
Taarifa zimeeleza kuwa makumi ya watu wameendelea kupata matibabu katika hospitali kadhaa jijini humo. Chopa (helicopters) za jeshi la nchi hiyo zimetumika kuwasambaza majeruhi katika hospitali hizo.
Aidha, imeripotiwa kuwa barabara mbovu za hatari, uzembe wa kutengeneza magari na uendeshaji wa hovyo umeendelea kuwa tatizo pia nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na gazeti la Dawn la Pakistan, takribani magari sita na pikipiki 12 pia ziliteketea kwa moto huo.