Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dkt. Grace Magembe ametoa siku tatu kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega kuwasilisha kwa Katibu Mkuu OR TAMISEMI, taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo Afya, Ujenzi wa jengo la Halmashauri na Elimu.
Dkt.Grace ameyasema hayo wakati wa ziara yake Wilayani humo na kubaini Halmashauri hiyo imepokea sh. Bilioni 2 za ujenzi wa Jengo la Utawala, sh. milioni 500 za ujenzi wa Hopsitali ya Wilaya, sh. milioni 500 za ujenzi wa vituo viwili vya Afya, sh. milioni 150 za ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashsuri na sh. milioni 200 za umaliziaji wa maboma ya zahanati.
Miradi yote hiyo bado haijatekelezwa na hivyo kuwakosesha wananchi huduma za muhimu na pia kuwafanya watumishi wa Halmashauri hiyo kufanya kazi kwenye mazingira magumu kwa sababu ya ukosefu wa ofisi na mahitaji mengine muhimu.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Kiomoni Kibamba amesema ni kweli fedha zipo lakini kumekuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinakwamisha kuanza kwa miradi hiyo muhimu na kuahidi kuwasilisha taarifa hiyo ndani ya siku tatu ikiwa na mikakati ambayo itawezesha miradi yote kuanza haraka iwezekanavyo.