Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi – CCM, Daniel Chongolo amewahakikisha wananchi wa Mkoa wa Katavi kuwa Chama hicho kitasimamia upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa maeneo ya mkoa huo, utakaopatikana kwa kuunganishwa na gridi ya taifa.
Akizungumza na Wanachama, Viongozi wa CCM na Wananchi wa Mpanda Mjini, Jumatatu Oktoba 2, 2023 katika ofisi za chama hicho Mkoa wa Katavi, mara baada ya kuwasili mkoani humo, kuanza ziara ya kikazi, Ndugu Chongolo ametumia nafasi hiyo kuzungumzia changamoto ya kukosekana kwa umeme wa kutosha katika mkoa huo kutokana na kutounganishwa na gridi ya taifa.
Amesema, “suala la kuunganisha umeme wa gridi ya taifa kutoka Tabora kuja Mpanda, ujenzi wa vituo va kupoza umeme tayari vimeshamilika. Lakini umeme wa kupokelewa ili upozwe ndiyo haupo. Subira imekuwa ndefu.Nimeambiwa viongozi kadhaa wamekuja kuelezea hilo na kutoa maelekezo kadhaa na maagizo ili Mpanda na Nkasi wapate umeme wa uhakika.
“Kigoma wameshaunganisha kwa sehemu kubwa ya mkoa, Rukwa tayari bado Mkoa wa Katavi. Niwaahidi ninatamani kuchaguliwa kwa kishindo katika mkoa huu Chama Cha Mapinduzi , ni matamanio yangu hayo ni kutokuwa na ahadi hewa itakayotusumbua au kutupatia maswali huko mbele.” amesema Chongolo.
Aidha, amewaeleza Wananchi hao kuwa atazungumza na Waziri wa Nishati, ili kupata ufumbuzi wa jambo hilo.“Nitawaita wanaohusika na hili jambo , huu mradi unafanywa na TANESCO kwani watu wengi wanataka kuwekeza katika viwanda vikiwemo vya kuchakata alizeti na tumbaku lakini changamoto ni umeme wa uhakika.