Wazazi na walezi nchini wametakiwa kufanya tathimini juu ya fursa na changamoto zilizopo katika familia zao hususani kipindi hiki ambacho jamii inakabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona, bila kuwanyanyapaa waliopata maambukizi.
Wito huo umetolewa leo jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizungumza kuhusu Siku ya Familia Duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 15 ya Mwezi Mei.
Ameziasa familia zisiwanyanyapae waliopata maambukizi ya Corona kwani ni tabia ambayo inaweza kupunguza upendo na utu miongoni mwa Watanzania wakati huu wa mapambano dhidi ya COVID-19.
“Niwaombe wazazi na walezi muwe karibu na familia zenu hasa watoto na wazee na punde mnapobaini dalili za ugonjwa wa Corona watoe taarifa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa” amesisitiza Ummy.
Amesema kutokana na umuhimu wa familia kwa ustawishi wa jamii, Wazazi na walezi wana kila sababu ya kubadilisha tabia, mitazamo na kuongeza maarifa huku wakiongeza mbinu za kuiwezesha familia kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo maambukizi ya Virusi vya Corona.
Aidha amesisitiza wazazi na walezi kuhakikisha wanatumia kipindi cha mapambano dhidi ya Corona kuwa karibu na familia zao huku wakifanya ufuatiliaji wa karibu hasa kwa watoto na Wazee kwa kufuatilia hali zao za lishe na endapo kuna mabadiliko wachukue hatua stahiki ya kutoa taarifa na kuwapeleka Katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Tanzania inaungana na Mataifa mengine ulimwenguni kila tarehe 15 mwezi Mei kuadhimisha Siku ya Familia Duniani ambayo kwa Mwaka huu inaongozwa na Kauli Mbiu isemayo “Familia ni Msingi katika kutokomeza Corona, tuilinde na tuwalinde wengine”