Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya usafirishaji bidhaa baharini, ambayo huadhimishwa kila alhamisi ya mwisho ya mwezi Septemba, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema meli zitakazosafiri katika muongo huu zitatoa majibu iwapo sekta ya usafirishaji imejipanga kutotoa hewa chafuzi ifikapo mwaka 2050.

Sambamba na hatua hiyo, pia itasaidia kutoa majibu ya usalama wa usafirishaji iwapo inazingatia hali ya usalama na usambazaji wa hewa chafuzi ambazo zinatajwa kuchangia kwa asilimia kubwa katika mabadiliko ya hali ya hewa na maradhi kwa binadamu.

Guterres ameyasema hayo katika ujumbe wake wa siku ya usafirishaji hii leo Septemba 29, 2022 ambayo maudhui yake ni teknolojia mpya kwa usafirishaji majini usiochafua mazingira na kusema “meli janja na zisizotoa kabisa hewa chafuzi lazima ziwe ndio chaguo la kawaida na ziwe zinapatikana kibiashara kwa watu wote ifikapo mwaka 2030.”

Miongoni mwa vyombo vinavyoshutumiwa kutoa hewa chafuzi katika sekta ya usafirishaji. Picha na Jing Zhang/ UN

Amesema, hatua hiyo ni muhimu kutokana na ujumbe wa mwaka huu unamulika umuhimu wa majawabu ya usafirishaji baharini endelevu, majawabu ambayo yatapunguza utoaji wa hewa chafuzi ikiwemo hewa ya ukaa, majawabu yatakayolinda mazingira na kuhakikisha kiwango cha joto hakizidi nyuzi 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi kwa mujibu wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, usafirishaji majini huchangia zaidi ya asilimia 80 ya biashara duniani na kwamba vita ya Ukraine na Mkataba wa Bahari Nyeusi wa kusafirisha nafaka, vimekumbusha jukumu muhimu la usafirishaji majini na lishe kwa dunia na kudai kuwa bila hatua za pamoja, kiwango cha hewa chafuzi kutoka katika sekta ya usafirishaji majini kinatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 230 ifikapo mwaka 2050.

Mpango udhibiti magonjwa yatokanayo na wanyama waiva
MCT yapongeza uwasilishwaji muswada Bungeni ulinzi wa data