Benki ya Exim sambamba na wafanyakazi wa benki hiyo hii wiki hii walikabidhi msaada ya vyakula kwenye vituo vinne vya kulelea watoto yatima na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu vilivyopo katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga na Mjini Magharibi – visiwani Zanzibar.

Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unaotekelezwa na benki hiyo unaofahamika kwa jina “Exim Cares”. Kwa mujibu wa uongozi wa Benki hiyo, msaada huo ulilenga katika kushiriki katika kuwapa faraha zaidi watoto hao hususan katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Eid.

Kwa upande wa jiji la Dar es Salaam, zoezi hilo liliongozwa na Mkuu wa Idara Masoko na Mawasiliano wa benki hiyo, Stanley Kafu. Akiwa kwenye kituo cha kulelea watoto yatima cha Malaika Kids, kilichopo wilayani Kinondoni, Kafu alitumia fursa hiyo kuwasisitiza watoto wanaoishi kwenye vituo hivyo kusoma kwa bidii kwa kuwa taifa linategemea mchango wao katika kufanikisha maendeleo.

Msaada huo ulihusisha vyakula vya aina mbalimbali ikiwemo mchele, mafuta ya kupikia, sukari, maharage pamoja na vinywaji .

“Zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya kusherehekea Sikukuu ya Eid Ul Fitr, Benki ya Exim tuliona ni vema tusherehekee pamoja na watoto yatima pamoja na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu kwa kuwapatia mahitaji haya muhimu ili na wao waweze kufurahia siku hiyo muhimu kama wenzao waliopo majumbani…tunashukuru wametupokea vizuri na wameonyesha kufurahishwa na hilo,’’ alisema.

Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya Exim Tanzania wakishusha msaada ya vyakula  kwa walezi  wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Malaika Kids kilichopo Wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo, Mlezi wa kituo hicho Bi Neema Mohamed aliishukuru benki hiyo kwa wema huo huku akitoa wito kwa taasisi nyingine pamoja na watu binafsi kujitokeza pia ili kusaidia watoto wanaoishi kwenye vituo hivyo kwa kuwa mahitaji bado  ni makubwa.

Angalia picha zaidi:

Meneja Mwandamizi wa benki ya Exim Zanzibar, Mwinyimkuu Ngalima ( wa tatu kushoto) sambamba na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi,Ali Hassani (katikati) wakikabidhi msaada ya vyakula  kwa walezi na watoto wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Muzdalifah Charitable Organization kilichopo mjini humo
Meneja Msaidizi wa benki ya Exim Mtwara Bw John Kayombo (alieketi) pamoja na wafanyakazi wengine wa benki hiyo wakiwa kwenye picha ya pamoja na walezi pamoja na watoto wa kituo cha kulelea watoto yatima cha EAGT Rahaleo Orphanage Centre kilichopo mkoani  humo baada ya kukabidhi msaada wa vyakula kwa watoto hao.
 
Meneja Msaidizi  wa benki ya Exim Mtwara, John Kayombo (kushoto)  akikabidhi msaada ya vyakula  kwa watoto wa kituo cha kulelea watoto yatima cha EAGT Rahaleo Orphanage Centre kilichopo mkoani humo
Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya Exim jijini Tanga wakiwa kwenye picha ya pamoja na walezi pamoja na watoto wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Goodwill Orphanage kilichopo jijini humo baada ya kukabidhi msaada

Rais wa Zambia afungua mpaka na Tanzania
Wanne wamwaga wino Msimbazi