Baadhi ya Mashabiki wa Tabora United ya mkoani Tabora inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2023/24 wameonyesha kutoridhishwa na matokeo ya timu yao.
Hali hiyo imejitokeza baada ya mchezo dhidi ya Geita Gold uliopigwa mwanzoni mwa juma hili katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Nyankumbu mkoni Geita na kumalizika kwa suluhu.
Shabiki anayejulikana kwa jina la Juma Salum, amesema haelewi ni kwa nini timu yao inashindwa kupata ushindi, hali ambayo inaendelea kuididimiza timu hiyo kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
“Sisi kama mashabiki wa Tabora United ni lazima tuulize uongozi shida iko wapi, ni wachezaji au ni mwalimu, na kama tatizo ni la viongozi tujue nani wanasababisha hadi wachezaji wanakosa morali ya kupambana,” Juma amesema.
Naye Haruna Msoga, amesema kutoka sare hasa ugenini si mbaya, lakini wanawataka viongozi wao kuongeza nguvu katika kipindi cha dirisha dogo ili kuhakikisha mzunguko wa pili wanakuwa imara na kufanya vyema.
“Hiki ndicho sijakielewa, kama tunatoka sare nje, basi tukija nyumbani tuwe tunashinda wapinzani wanapataje sare hapa. lazima tukae chini na kufahamu wapi kuna tatizo, hatutaki kusubiri mambo yaharibike zaidi?” amehoji Abdulrahman Slim.