Simba imeanza michuano ya Mapinduzi kwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Jamhuri ya Pemba katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
Simba ambao ni mabingwa watetezi wa kombe hilo walipanga kikosi cha wachezaji wengi ambao wamekuwa hawapati nafasi ya kucheza katika mechi za Ligi Kuu Bara na walionekana kutoelewana vizuri kabisa.
Pasi nyingi kwa Simba hazikuweza kuisaidia ingawa ilianza kupata bao la kwanza mapema tu kupitia kwa Awadhi Juma aliyelipa shuti kali nje ya 18, hiyo ilikuwa ni dakika ya 12.
Lakini Jamhuri wakasawazisha dakika chache baadaye kupitia kwa Mwalimu Mohammed katika dakika ya 18 aliyefunga kutokana na safu ya ulinzi ya Simba kuonekana kujichanganya huku Jonas Mkude na Mohammed Fakhi wakionekana kutoelewana.
Jamhuri ilipata bao la pili kupitia kwa Ammy Bangekesa  katika dakika ya 52 mara tu baada ya kuanza kwa kipindi cha pili lililotokana na makosa mengine ya Fakhi kabla ya Awadhi Juma kufunga bao la kusawazisha kwa Simba katika dakika ya 76.
Kutokana na wachezaji wengi wa Simba kuboronga, Kocha Dylan Kerr aliamuwa kuwaingiza Hamisi Kiiza, Dani Lyanga, Ibrahim Ajib na Mwinyi Kazimoto ambao waliiwezesha Simba kutawala mchezo zaidi.

Serikali Yanunua Mashine Mpya Ya CT-Scan Muhimbili
Benitez Afungashiwa Virago Real Madrid