MCHEZO wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya wenyeji Simba dhidi ya Dodoma Jiji, uliokuwa uchezwe majira ya Saa 1 Usiku, sasa umerudishwa nyuma.
Katika mchezo huo namba 132 wa Ligi, utakaochezwa kesho Jumatatu, sasa utachezwa mapema saa 10 jioni katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, badala ya kuchezwa saa 1 usiku kama ratiba ya awali ilivyokuwa imepangwa.
Licha ya taarifa kutowekwa wazi, lakini pasina shaka ni kwamba, sababu zilizotajwa kupelekea mchezo huo kubadilishwa muda ni kupisha ukarabati wa kangavuke la ndani ya uwanja wa Mkapa litakalofanyika baada ya mchezo.
Tayari klabu zote mbili zimeshajulishwa kuhusu mabadiliko hayo, ikiwemo wageni Dodoma Jiji ambao wao wamesema hawana jinsi kwa kubadilika kwa muda huo wa mchezo, japo imewasumbua kiasi.
Mtendaji wa timu hiyo, Fourtnatus Johnson anakiri kwamba “Mabadiliko tumeyapokea kutoka kwa bodi ya Ligi na sababu zilizotajwa haziepukiki japo kwetu imekua changamoto sana kwa mchezo wa pili huu tunabadilishiwa muda wa mchezo” alisema Johnson.
Mtendaji huyo aliongeza, “mchezo uliopita (Ruvu Shooting) tulibadilishiwa muda kwenye kikao cha maandalizi ya mechi, kama timu hatuna budi kuyapokea na haya dhidi ya Simba, tupo kamili kwa mchezo huo katika huo muda mpya” alisisitiza Mtendaji huyo