Kocha msaidizi wa timu ya Simba, Masoud Djuma, amesema kuwa wachezaji wa timu yake wamejiandaa kushinda mchezo wa fainali wa mashindano ya SportPesa Super Cup dhidi ya Goh Mahia ili waweze kufika Uingereza kwa mara ya kwanza.
Djuma amesema hayo wakati akiongea na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa fainali wa mashindano ya Super Cup dhidi ya Goh Mahia leo nchini Kenya na kuongeza kuwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi wa timu ya Simba hawajahi kufika Uingereza hivyo ni mchezo wa leo ndiyo njia ya kufika Ulaya.
“Kwanza sisi sote hakuna ambaye amefika Uingereza, ukianzia kwangu nilifika Uingereza lakini niliishia uwanja wa ndege, hapo sio kufika maana sikuingia mjini, mnajua hamu niliyo nayo pamoja na ile ya wachezaji,” amesema Djuma.
Aidha, Kocha huyo ameongeza kuwa katika mchezo wa leo watacheza vizuri zaidi kuliko michezo miwili iliyopita ambapo timu yake haikufanikiwa kufunga goli hata moja na kuongeza kuwa hiyo ilitokana na wachezaji kutozoea mfumo mpya baada ya kutambulisha wachezaji wageni katika timu.
Hata hivyo, timu ya Simba inapambana na klabu ya Goh Mahia kutoka Kenya katika mchezo wa fainali wa mashindano ya SportPesa Super Cup ambapo mshindi wa mchezo huo ataenda nchini England kucheza na klabu ya Everton.
Mchezo huo wa fainali utapigwa katika Uwanja wa Afraha nchini Kenya kuanzia saa 9:00 Alasiri.