HARAKATI za kuwania taji la Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara, zitaendelea tena leo kwa vinara wa msimamo wa Ligi hiyo Simba Queens kuwakaribisha mabingwa watetezi JKT Queens kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena ulioko Bunju jijini, Dar es Salaam.
Simba Queens wenye alama 35 watashuka dimbani wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao kumi kwa sifuri walioupata ugenini dhidi ya Ruvuma Queens, wakati JKT Queens wenye alama 29 wao waliiadhibu Tanzanite Queens magoli kumi na mbili kwa sifuri.
Kocha Mkuu wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’, amesema wamejipanga kuendelea kutoa ‘dozi’ ili wafikie malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa mara ya kwanza msimu huu.
Mgosi amesema anafahamu mechi hiyo itakuwa na ushindani, lakini wachezaji wake wamejiandaa kuonyesha ubora wao.
“Sisi kila mechi kwetu ni sawa na fainali, tutaingia uwanjani kwa tahadhari ili tukicheza kwa umakini, hakuna mechi rahisi msimu huu, kila timu ina malengo yake,” Amesema Mgosi.
Naye Nahodha wa Simba Queens, Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’, amesema wachezaji wote wamejiandaa vizuri kuelekea mchezo huo na wamejipanga kuondoka na pointi tatu muhimu.
Gaucho amesema wanataka kupata ushindi ili kuwafurahisha mashabiki wao kama walivyofanya ‘kaka’ zao kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara. Michezo mingine Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara itakayochezwa leo ni kati ya Alliance Girls dhidi ya Panama Girls wakati Baobab Queens wanawakaribisha Marsh Queens huku Yanga Princess wanawafata Mlandizi Queens kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi, mkoani Pwani.